VIEW OTHER SITES

Friday

BOLT ASHINDWA KUVUNJA REKODI YAKE CZECH



Mwanariadha mjamaica, Usain Bolt hii leo amefanikiwa kushinda mbio za mitaa 100 zilizofanyika Golden Spike, Ostrava,Jamhuri ya Czech.
Katika mbio hizo kuelekea mashindano makubwa ya olimpiki jijini London yalishuhudiwa kwa Bolt kushiriki kwa mara ya sita katika mbio zilizofanyika kwenye mji huo ambapo alishinda kwa sekunde 10.04.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Bolt kwenye ardhi ya Ulaya kuelekea mashindano ya Olimpiki, kwa upande mwingine nafasi ya pili ilienda kwa Kim Collins raia wa visiwa vya St. Kitts na Nevis aliyetumia sekunde 10.19, akifuatiwa na Darvis Patton wa Marekani aliyetumia sekunde 10.22.
Hata hivyo Bolt alishindwa kuvunja rekodi yake ya sekunde 9.82 aliyoiweka mwanzoni mwa mwezi Mei nchini Jamaica.
Bolt ni mshindi wa medali tatu za dhahabu kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika 2008 Beijing, Japan.

OKWI ATAKIWA AUSTRIA


MSHAMBULIAJI wa Simba SC na raia wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi anaweza kuuzwa na klabu yake kwa moja ya klabu za nchini Austria kwa gharama ya dola za Kimarekani 500,000    (sawa na Sh. Milioni 750 za Tanzania) na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyewahi kuuzwa kwa bei ghali zaidi ndani ya klabu ya Simba SC.

Rekodi hiyo inashikiliwa na Mbwana Ally Samatta aliyeuzwa kwa dola za Kimarekani 100,000 kwenda klabu ya Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) msimu uliopita.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu ya Simba, ambazo blog hii imezipata zinasema kwamba, Okwi mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, mwenye umri wa miaka 19 aliyetua Msimbazi msimu wa 2010 akitokea klabu ya SC Villa ya Uganda anatakiwa na klabu hiyo kwa dau hilo.

Ofa hiyo tayari iko mezani kwa Simba na kwa sasa inafanyiwa kazi kabla ya wakati wowote kutangazwa rasmi kuuzwa kwa mchezaji huyo, aliyesajiliwa na Wekundu wa Msimbazi, kwa dau la dola za Kimarekani 5000.

MAANDALIZI YA UMISSETA MWANZA YASHIKA KASI


Maandalizi ya mashindano ya UMISSETA mwaka huu kwa ngazi ya mkoa wa Mwanza yazidi kupamba moto kwenye shule ya sekondari Nsumba ambapo ni kituo cha mashindano hayo kwa mkoa wa Mwanza.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufungua pazia lake mnamo Juni,2 kwa kushirikisha wilaya zote za mkoa wa Mwanza, miongoni mwa michezo itakayohusika ni pamoja na soka, pete, kikapu, wavu, riadha, tenisi, mikono na bao.
Akizungumzia mashindano hayo, mratibu wa UMISSETA kanda, Kabuche Suleiman Enock Shaibu amesema kuwa, maandalizi ya mashindano ya mwaka huu yako vizuri na wanatarajia upinzani baina ya wilaya zitakazoshiriki mashindano ya mwaka huu kutokana na maandalizi yao.
Lakini pia ameelezea changamoto wanazokutana nazo ikiwemo vifaa vya mchezo ikiwemo mipira huku akitoa amasa kwa wadau wa michezo kijitokeza kuwezesha mashindano hayo yafanyike kwa ustadi zaidi, hata hivyo UMISSETA kwa sasa jiji ndilo linajitoa zaidi kusaidia mashindano hayo.
Wilaya zitakazoshiriki mashindano ya mwaka huu ni Nyamagana, Ilemela, Magu, Misungwi, Kwimba, Sengerema, Ukerewe na Geita.

Twiga stars yawasili Ethhiopia bila Mwasikili


Kikosi cha timu ya taifa ya wanawake nchini, Twiga Stars kimefika salama nchi Ethiopia tayari kuikabili timu hiyo kwenye mchezo wa mchujo ili kupata nafasi ya kushiriki kombe la mataifa ya Afrika 2012 yatayofanyika nchini Guinea ya Ikweta.
Kikosi kilicho chini ya kocha mzawa, Charles Boniface Mkwasa imefikia hoteli ya Churchill jijini Addis Ababa baada ya kuwasili saa moja na nusu sawa na saa mbili na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Mchezo huo utapigwa tarehe 27 mwezi huu kwenye uwanja wa Addis Ababa, awapo awali Twiga Stars waliitoa timu ya taifa ya Namibia kwa jumla ya magoli 7-2.
Hata hivyo Twiga stars watamkosa beki Sofia Mwasikili ambaye klabu yake ya nchini uturuki haijamwachilia kwa mcezo huo utakaopigwa jumapili hii.

NCHUNGA: KULIKUWA NA HALI YA USALITI KLABUNI


MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ametangaza kujiuzulu wadhifa wake ofisini kwake, jengo la NSSF, barabara ya Bibi Biti, Dar es Salaam, baada ya kuvamiwa na kundi la watu nyumbani kwake, Mbezi, Jijini usiku wa wa manane.
Lakini Nchunga amekataa kulihusisha tukio hilo na kujiuzulu kwake, akisema kwamba amefikia uamuzi huo ili kuinusuru Yanga, kwa sababu wapo watu ambao wako tayari Yanga ife, lakini wamng'oe yeye madarakani, kitu ambacho yeye hataki kitokee.
Nchunga alisema kuwa majira ya saa nane usiku, alivamiwa na kundi la watu takribani 15, lakini hawakufanikiwa kufanya chochote kutokana na ulinzi mkali uliopo katika nnyumba hiyo.
"Kwanza mbwa walianza kubweka, walinzi wakashituka wakaomba msaada kwa walinzi wenzao, nasi tukapuga simu polisi, wakaja haraka sana na kukuta watu hao wamekwishakimbia,"alisema

TAARIFA YA KUJIUZULU KWA NCHUNGA:

LLOYD NCHUNGA BIHARAGU
C/O LLOYD ADVOCATES,
Morogoro/Bibi TIti  Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers
P.BOX 75111, Dar-Es- Salaam,Tanzania.


                                                                   

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA KLABU YA YANGA.
Ndugu wana Habari, najua kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klabu, kwa wajumbe wa kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo.
Tangu tumeingia madarakani tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa wa  Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tulifuta uteja kwa watani wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei 2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika klabu yetu.
Hali kadhalika tumeshirikiana  mpaka tumeweza kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia mkataba na  kampuni ya NEDCO  kuendeleza mali zetu katika mtaa wa mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati miliki za maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za mwisho za kumalizia michoro.
Hali kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na kukusanya data za wanachama na kusajili  wapya tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu. Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
Kwa ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano kwa kiongozi ajaye.
Aidha, tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa, na kongamano la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.
Haya yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo mtaona yalikuwa mazuri.
Lakini pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja.  Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu  ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali, tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.
Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa  mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema.
Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k.  Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo  tuvune bao 5!
Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali.
Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia.
Baada ya mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao , Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo  cha Redio moja maarufu hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza!
Hii imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu.
Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti  wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu.
Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi.
Natumaini kamati ya utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa  mafanikio zaidi.
 Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa  na uwezo wa kufanya hivyo.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.
Wasalaam,


LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.
Nakala kwa:-
Mama Fatma Karume,Mdhamini
Francis Kifukwe, Mdhamini
Bwana Yusuf Manji – Kwa taarifa

MATOKEO MECHI ZA KIRAFIKI ZA KIMATAIFA NA LIGI KUU ZIMBABWE



Georgia   1 - 3     Turkey    Salzburg
Japan     2 - 0     Azerbaijan    Shizuoka
Peru 1 - 0     Nigeria   Lima
El Salvador   2 - 2     New Zealand   Houston
Venezuela 4 - 0     Moldova   Puerto Ordaz

Zimbabwe 2012 / 2013

Chicken Inn   1 - 0     Black Mambas  Rufaro
Harare City   0 - 1     Buffaloes Mucheke
Gunners   2 - 1     Hardbody  Motor Action Sports Club
CAPS United   3 - 1     Platinum  Luveve

GUARDIOLA KUFUNGA KAZI NA BARCELONA LEO


Klabu ya FC Barcelona wataikabili Athletic Bilbao hii leo kwenye mchezo wa fainali ya kombe la mfalme nchini uhispania utakaopigwa umanja wa Vicente Calderon jijini Madrid.
Kocha Pep Guardiola atakalia benchi la ufundi la klabu hiyo kwa mara ya mwisho kuiongoza Barcelona kwenye mchezo huo wa fainali ya 7 dhidi ya Bilbao.
Barcelona imetwaa mataji 25 ya kombe la mfalme akifuatiwa na Bilbao iliyotwaa mara 23, kati ya mara 6 ilizokutana Barcelona wameshinda mara 4 huku Bilbao wakishinda mara 2.
Fainali hii itampatia taji la 14 Guardiola endapo Barcelona watashinda dhidi ya Bilbao iliyocheza kwa mara ya mwisho 1984.
Barcelona wataingia uwanjani bila ya Puyol, Abidal na beki wa kulia, Dani Alves atakayekuwa nje kwa majuma sita hadi nane baada ya kuumia mguu wa kulia akiwa mazoezini huku Bilbao walio chini ya Muargentina, Marcelo Bielsa wataingia wakiwa na mshambuliaji wao wa kutumainiwa, Fernando Llorente Torres mwenye magoli matano kwenye ligi hiyo. Vikosi vitakavyochuana hii leo,
BILBAO:Iraizoz;Iraola, Martinez, Amorebieta, Aurtenetxe;
De Marcos, Iturraspe, Herrera;Susaeta, Llorente, Muniain
BARCELONA:Pinto;Montoya, Pique, Mascherano, Adriano;Xavi, Busquets, Iniesta;Fabregas, Messi, Alexis.