VIEW OTHER SITES

Tuesday

RUVUMA YAIADHIBU KIGOMA COPA COCA COLA


Timu ya mkoa wa Ruvuma imeanza vizuri michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuifunga Kigoma ambayo ni bingwa mtetezi kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kundi A uliofanyika hivi leo asubuhi (Juni 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Kigoma ambayo iliifunga Lindi mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa juzi, ilishindwa kufua dafu mbele ya Ruvuma na kuruhusu bao katika kila kipindi.
Mabao yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Edward Songo. Mshambuliaji huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 34 wakati la pili alilipachika dakika ya 84.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi, Tanga na Morogoro zilitoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mkoani Pwani, Mara iliifunga Temeke bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu wakati Kagera ililala bao 1-0 mbele ya Kilimanjaro katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tamco.
Aidha, TFF itawazawadia wapiga picha za magazetini watakaoripoti mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 ngazi ya Taifa yanayoendelea kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca-Cola na kushirikisha mikoa 28 yanafanyika viwanja vya Tanganyika Packers, Kumbukumbu ya Karume mkoani Dar es Salaam, na viwanja vya Tamco na Nyumbu mkoani.
Zawadi ya sh. 250,000 itatolewa kwa picha bora katika maeneo matatu; action picture, fair play picture na mpiga picha ambaye ameripoti matukio mengi ya mashindano hayo yanayoshirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17. Washiriki wanatakiwa kuwasilisha picha zao zilizotumika (cuttings) TFF.

NGORONGORO HEROES YAPATA KOCHA MPYA


SHIRIKISHO la Soka Tanzania nchini (TFF) limemtambulisha rasmi kocha mpya wa timu za Taifa za vijana, Jakob Michelsen kutoka Denmark  hii leo mbele ya waandishi wa habari ambaye anachukua nafasi ya Kim Poulsen ambaye hivi sasa anakinoa kikosi cha wakubwa Taifa Stars.
Michelsen ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja alitambulishwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na kusema falsafa yake ni kama ile ya Poulsen ya kumiliki mpira na kushambulia muda wote wa mchezo.
Kabla ya ujio wake Tanzania, Michelsen alikuwa kocha wa timu ya daraja la kwanza ya Hobro IK ya Denmark. Ana leseni A ya ukocha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya ukocha wa vijana kutoka Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).
Moja ya mafanikio yake ni kuipa ubingwa wa Denmark, timu ya Skovbakken kwenye ligi ya timu zenye umri chini ya miaka 18. Ubingwa huo aliupata msimu wa 2005/2006.