Rais wa Brazil Dilma Rousseff amesaini kuwa sheria
muswada utakaoruhusu uuzwaji wa bia wakati wa mechi za Kombe la Dunia mwaka
2014.
Shirikisho
la Soka Duniani, Fifa, lilikuwa likitaka kufanyiwa mabadiliko katika sheria ya Brazil inayopiga
marufuku pombe kuuzwa kwenye viwanja vya mpira wa miguu.
Muswada
huo mpya umepitisha sheria kadhaa kwa ajili ya Kombe la Dunia, haujaelezea
kuweka pingamizi lolote la kuuzwa pombe, uuzaji wa pombe ulikuwa mwiko katika
mechi za kandanda nchini Brazil tangu mwaka 2003.
Upigwaji
huo marufuku uliwekwa ikiwa ni sehemu ya hatua ya kupambana na vurugu miongoni
mwa mashabiki wa timu zenye uhasama pamoja na kukabiliana na wahuni.
Mwanzoni
mwa mwaka huu Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke, aliweka bayana kwamba haki ya
kuuza pombe ni lazima irejeshwe kuwa sheria wakati wa michuano ya Kombe la
Dunia kwenye Bunge la Brazil.
Wakati
wa ziara ya kukagua viwanja kwenye miji 12 ya Brazil itakayochezewa mechi hizo,
alionesha hisia zake kwa jambo hilo.
"Unywaji
wa pombe ni sehemu ya patashika za Kombe la Dunia, kwa hiyo tutahakikisha
unaruhusiwa. Mtaniwia radhi iwapo nitakuwa nawakwaza kwa kiasi fulani lakini
hilo ni jambo ambalo halina mjadala," alisema.
Kampuni
ya bia ya Budweiser ndio wadhamini wakubwa wa Fifa.

