VIEW OTHER SITES

Sunday

STARS YAANZA KUJIFUA IKIWA IVORY COAST


Timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeanza kujifua ikiwa Ivory Coast kujiandaa na mechi ijayo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2014 nchini Brazil, dhidi ya Gambia itakayochezwa Jumapili ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha Mdenmark, Kim Poulsen, leo aliiongoza Taifa Stars kufanya mazoezi asubuhi kwenye uwanja wa Shirikisho la Soka la Ivory Coast (FIF) pembezoni mwa jiji la Abidjan.
Timu hiyo itafanya tena mazoezi kesho (Juni 4 mwaka huu) asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani saa 1.30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Dar es Salaam, Juni 5 mwaka huu saa 1.40 asubuhi.
Kocha Kim aliwakosa wacheaji wanne ambao ni majeruhi (Thomas Ulimwengu, Nurdin Bakari, Haruna Moshi na Nassoro Masoud Cholo) amesema hivi sasa wameelekeza mawazo yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Gambia.
“Safari ya kujenga timu ndiyo imeanza. Mechi dhidi ya Ivory Coast imepita na ninawashukuru wachezaji kwa kucheza kwa mujibu wa maelekezo na kujituma. Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa yaliyosababisha tuwape Ivory Coast mabao mepesi.
“Lakini kama nilivyosema mechi hiyo imepita, hivi sasa tunaangalia mechi ijayo dhidi ya Gambia. Hatuna muda mwingine wa kujipanga na ndio maana niliamua kuja na wachezaji wote Abidjan,” amesema Kim.
Mechi dhidi ya Gambia itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Gambia ilitoka sare ya bao 1-1 na Morocco katika mechi iliyochezwa juzi jijini Banjul.
Taifa Stars itamkosa na nahodha msaidizi, Aggrey Morris aliyeoneshwa kadi nyekundu dakika ya 65 baada ya kupata ya pili ya njano kwenye mechi dhidi ya Ivory Coast iliyochezwa Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny jijini Abidjan.

No comments:

Post a Comment