Uongozi wa Twiga Stars umekana kuwepo vitendo vya kinyume na
maadili kwa wachezaji wa timu hiyo ambayo hivi karibuni ilitolewa kwenye mechi
za mchujo za michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC).
Wakizungumza na waandishi wa habari leo, Meneja wa Twiga
Stars, Furaha Francis na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Charles Boniface
Mkwasa wamesema hakuna vitendo vya aina hiyo.
Mkwasa amesema alikaririwa vibaya kuhusu suala hilo wakati
akiwa kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha Star Tv kutokana na swali
alilokuwa ameulizwa kuhusiana na vitendo hivyo.
“Ukifuatilia mahojiano yangu na Star Tv mimi sikusema kuwa
kuna vitendo hivyo. Tatizo nadhani lilianzia kwa magazeti yaliyonukuu kupitia
Star Tv, na wala kujiuzulu kwangu hakukuhusiana na hilo, nimewajibika kama
kocha kutokana na kutolewa na Ethiopia,” amesema Mkwasa.
Naye Furaha Francis amesisitiza kuwa hakuna vitu vya aina
hiyo katika timu hiyo, na kama kuna mtu ana ushahidi na hilo ni bora akauonesha
badala ya kuzungumzia uvumi kuliko ukweli.
“Ukweli ni kwamba si sisi na wachezaji tu ambao
hatukufurahishwa kutolewa na Ethiopia, wapo Watanzania wengi ambao
hawakufurahishwa na matokeo yale. Twiga Stars si timu ya kudumu, haikai na
wachezaji kwa muda wote, kila mchezaji ana timu yake.
“Madai yanayoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu
vitendo hivyo yametuchafua sana. Tunaomba kama kuna mtu ana ushahidi na hilo
atueleze kuliko kuendelea kutuchafua,” amesema.

No comments:
Post a Comment