Kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima "Fabregas" amerejea jana usiku na kujiunga na kikosi cha Mabingwa wa Afrika
Mashariki na Kati, Young Africans Sport Club (YANGA) katika mazoezi
yaliyotarajiwa kuanza leo jioni saa kumi katika uwanja wa Kaunda Jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza na tovuti ya klabu www.youngafricans.co.tz kiungo
huyo amesema kuchelewa kwake kulitokana na matatizo binafsi yaliyomkuta wakati akiwa nchini kwao na kusababisha kuchelewa kujiunga na Kikosi
chake.
Haruna amewataka wachezaji wenzake kurejesha heshima kwa
mara nyingine kwa kutwaa kombe la Kagame katika michuano inayotarajiwa kuanza
Julai 14 Mwaka huu, huku Yanga ikiwa ndiyo Mabingwa watetezi wa michuano hiyo.
Niyonzima amesema tangu alipokuwa mapunziko alikuwa
akifuatilia kwa karibu juu ya Klabu yake ya Yanga hasa katika zoezi la usajiri
unaoendelea na kupongeza usajili huo kutokana na baadhi ya wachezaji
anaowafahamu kusajiriwa katika kikosi hicho.
Yanga itaanza kutupa karata yake dhidi ya Atletico ya
Burundi ambapo mechi hiyo ndiyo itakayokuwa ni pekee wakati wa ufunguzi
itachezwa katika uwanja wa Taifa,Jijini Dar es Salaam huku Simba ikaanza
kampeni siku inayofuata.
Mabingwa hao watetezi kundi lake limejumuisha na timu za Wau
Salaam ya Sudan,Altetico ya Burundi na APR ya Rwanda.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa BARAZA la vyama vya Soka Afrika
Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholous Musonye amesema mpaka sasa mdhamini ni
mmoja aliyejitosa kwenye michuano hiyo ambaye ni Rais wa Rwanda,Paul Kagame.
Jumla ya timu 12 zitashiriki katika michuano hiyo ambayo
itaanza Julai 14 hadi Julai 28 ambapo wawakilishi hao watatoka katika nchi za
Tanzania,Uganda,DR Congo,Djibout,Zanzibar,Kenya,Sudan Kusini,Rwanda na
Burundi.(Mwandishi wetu Louis Sendeu)

No comments:
Post a Comment