Timu ya mkoa wa Ruvuma(U-17) imefanya kweli hii leo katika
michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuishushia Lindi kipigo cha mabao 7-2
asubuhi ya leo.
Mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani
Pwani, washindi ambao kwa matokeo hayo wamejiweka katika nafasi nzuri ya
kucheza 16 bora walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
Waliotikisa nyavu ni Anthony Christian dakika ya 23 na 50,
Edward Songo dakika ya 27, 75 na 86 na Sunday Leonard dakika ya 32 na 60. Mabao
ya Lindi yalifungwa na Salum Mnyamwile dakika ya 18 kwa njia ya penalti na
lingine dakika ya 48 kupitia kwa Mwarami Maundu.
Nayo Tanga imepata ushindi wake wa kwanza katika michuano
hiyo baada ya kuifunga Manyara mabao 2-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa
Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Mabao ya washindi yalifungwa na Mbwana Musa
dakika ya 47 na Issa Mwanga dakika ya 60.
Tanga ilitoka sare ya mabao 3-3 na Morogoro, ikapata sare
nyingine ya 1-1 dhidi ya Mwanza.
Kagera imeendelea kujitutumua katika michuano hiyo baada ya
kupata ushindi wake wa pili katika kundi D kwa kuilaza Kusini Unguja bao 1-0
katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe jijini Dar es
Salaam.
Bao lake lilifungwa dakika ya 76 na Novati Sebastian. Mechi
iliyopita Kagera iliifunga Tabora mabao 2-0 baada ya kuteleza katika mechi
mbili za kwanza kwa kufungwa na Kilimanjaro na Singida.
Mechi nyingine ilichezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar
es Salaam ambapo Kinondoni iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mara.

No comments:
Post a Comment