VIEW OTHER SITES

Wednesday

MWINYI MGENI RASMI TUZO ZA TASWA


RAIS mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya awamu ya pili, Alhaji Ally Hassan Mwinyi, amechaguliwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za utoaji tuzo za wanamichezo bora Tanzania zitakazofanyika hapo kesho kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Abbas Pinto amesema hayo kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari mchana huu katika ukumbi wa City Sports Lounge, jijini Dar es Salaam na kwamba wamemchangua Mwinyi kwa sababu alikuwa ana mchango mkubwa katika sekta ya michezo enzi zake, akiwa Ikulu tangu 1985 hadi 1995 alipomuachia Benjamin William Mkapa.
Katika tuzo hizo, kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Fadhil Hakizimana Niyonzima wa Yanga, atachuana na Kipre Tchetche wa Ivory Coast anayechezea Azam FC na Mganda Emmanuel Okwi wa Simba kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa mwaka wa kigeni.
Kwa upande wa wanasoka wazalendo, tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka inawaniwa na John Bocco, Aggrey Morris, wote wa Azam na Juma Kaseja wa Simba, wakati kwa wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje wanaoshindana ni Henry Joseph wa Kongsvinger ya Norway na Mbwana Samatta wa Tout Puissant Mazembe ya DRC.
Kwa upande wa wanawake, Sophia Mwasikili anayecheza Uturuki, anashindana na Asha Rashid ‘Mwalala’, Mwanahamisi Omary wote wa Mburahati Queens, Fatuma Mustapha wa Sayari na Eto’o Mlenzi wa JKT.
Tuzo hizo zinadhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).

No comments:

Post a Comment