VIEW OTHER SITES

Wednesday

SIMBA, AZAM KUONESHANA UBABE LEO


Michuano ya Kombe la Urafiki inayondaliwa na Chama cha Soka Zanzibar(ZFA), inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mkali utakaowakutanisha mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC na Azam FC mabingwa wa kombe la Mapinduzi 2011/2012 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mchezo huo wa Kundi A unatarajiwa kuwa wa kusisimua kutokana na kiwango cha klabu ya Azam kilicho chini ya mwingereza, Stewart Hall huku kikiwa na nyota wa kiwango cha juu kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo Mrisho Ngassa, John Bocco bila kuwasahau Kipre Tcheche na nduguye Bolou.

Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kuwa wana matumaini ya kuifunga Azam FC leo.
Hata hivyo kwa upande wake, Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa amesema nao wako vizuri na wamejipanga vema kuifunga Simba SC.
Simba SC ilianza vyema baada ya kuifunga Mafunzo mabao 2-1, wakati Azam ililazimishwa sare ya 1-1 na U23, Karume Boys.
Mabao yote ya Wekundu wa Msimbazi yalitupiwa nyavuni na mshambuliaji mpya, aliyesajiliwa kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, Abdallah Juma, ambaye amepokewa Simba kama Emmanuel Gabriel mpya. Dullah alifunga mabao hayo dakika ya 27 na 44, yote akiunganisha pasi za kuingo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick Kanu Mbivayanga, wakati Mafunzo walipata bao lao kufutia machozi dakika ya 80, mfungaji Jaku Joma.
Azam wao juzi walilazimika kusubiri hadi dakika ya 79 kupata sare ya 1-1 kwa bao la mshambuliaji wake kutoka Ivory Coast, Kipre Tcheche, baada ya Karume Boys kupata bao la kuongoza dakika ya 45 kwa njia ya penalti, mfungaji Ibrahim Hamisi.
Katika mechi za kwanza za Kundi A jana, Yanga ya Dar es Salaam pia, ilifungwa kwa taabu mabao 3-2 na Jamhuri ya Pemba kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Yanga ambayo imepeleka wachezaji wake wa kikosi cha vijana visiwani humo, hadi mapumziko, ilikuwa tayari nyuma kwa mabao 2-1.
Lakini kipindi cha pili, Yanga B walikuja juu na kucheza soka ya kuvutia, ingawa waliishia kukosa mabao ya wazi kabla ya kupata moja na wapinzani wao wakipata moja zaidi pia .
Mabao ya Jamhuri yalitiwa kimiani na Ally Salum dakika ya 34, Abdallah Othman dakika ya 45 na Mohamed Omar dakika ya 69, wakati mabao ya Yanga yalifungwa na Hamisi Shaaban dakika ya 17 na Nofteli Mwansasu dakika ya 77.
Katika mchezo wa Kundi hilo uliotangulia hiyo jana, Super Falcon ilitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Zanzibar All Stars. Mabao ya Falcon yalifungwa na Deo Cassian dakika ya 12 na 25, wakati ya All Stars yalitupiwa nyavuni na Ahmad Malik dakika ya 46 na Twaha Mohamed dakika ya 81.

No comments:

Post a Comment