Kocha mpya wa Yanga,
Thom Saintfiet, kutoka Ubelgiji anatarajiwa kuwasili leo Dar es Salaam, tayari
kuanza kazi ya kukinoa kikosi cha mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame.
Ofisa Habari wa Yanga,
Louis Sendeu alisema jana kwamba, Thom aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa
Shirikisho la Soka Nigeria, akiwasili atakwenda moja kwa moja kufanya
mazungumzo na uongozi kwa ajili ya kusaini mkataba.
Alisema Saintfiet
ataanza kazi mara moja atakapowasili na kumaliza kusaini mkataba, ili kuiandaa
timu kwa ajili ya kutetea Kombe la Kagame, michuano inayotarajiwa kuanza Julai
14, mwaka huu, Yanga ikifungua dimba na mabingwa wa Burundi, Atletico.
Mbelgiji huyo anakuja
kurithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic aliyetupiwa virago mwishoni
mwa msimu.
Tangu kutupiwa virago
kwa Papic zikiwa zimesalia mechi tatu ligi kumalizika, Yanga imekuwa chini ya
Kocha wake Msaidizi, Freddy Felix Minziro.
Ujio wa Mbelgiji huyo,
unamaliza zama za makocha wa Kiserbia waliokuwa wakibadilishana uongozi wa
benchi la ufundi la Yanga, tangu mwaka 2007, kuanzia Milutin Sredojevic ‘Micho’
aliyewaachia Profesa Dusan Savo Kondic, Spaso Sokolovoski na Serdan Civojnov,
ambao nao walimuachia Papic.
Awali, Papic alipoondoka nafasi yake ilichukuliwa na Mganda, Sam
Timbe aliyeleta mataji mawili, ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Kagame, lakini
akarudishwa tena Mserbia huyo msimu uliopita kabla ya kutupiwa virago mwishoni
mwa msimu.

No comments:
Post a Comment