VIEW OTHER SITES

Saturday

TIKETI MECHI YA STARS KUUZWA LEO


Tiketi za mechi ya pili ya kufuzu kombe la dunia 2014 nchini Brazil kati ya Tanzania “Taifa Stars” na Gambia “Nge” zinaanza kuuzwa leo kuanzia majira ya saa 2 asubuhi kwenye vituo vya Mgahawa wa Steers uliopo mtaa wa Samora na Ohio, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Soko Kuu la Kariakoo na Uwanja wa Taifa.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo amesema kuwa mauzo yataendelea hadi siku ya mechi kwenye vituo husika kati ya saa 2 asubuhi hadi saa 6 mchana kisha kuhamia Uwanja wa Taifa.
Viingilio vya mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo ni 36,693 kati ya jumla ya viti 57,558 vilivyopo katika uwanja huo wa kisasa sawa na asilimia 63.7 ya watu watakaoshuhudia mchezo, viti vya rangi ya chungwa ni sh. 5,000, huku kwa upande wa VIP C watatozwa sh. 10,000 na VIP B itakuwa sh. 20,000. Kwa upande wa jukwaa la VIP A ambalo linachukua watazamaji 748 tu ambao ni asilimia 1.3 ya watu wote watalipia sh. 30,000.
Mechi hiyo itachezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itaanza majira ya saa 10 kamili jioni.
Msafara wa timu hiyo wenye watu 31 wakiwemo wachezaji 22 unaongozwa na
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo wa Gambia, Malang Jassey.
Viongozi wengine ni Ofisa Utawala wa timu, Modou Sowe, Kocha Luciano Mancini, makocha wasaidizi, Peter Bonu Johnson na Lamin Sambou, Kocha wa makipa Alhagie Marong, mtaalamu wa tiba ya mifupa, Pa Matarr Ndow, mtunza vifaa, Sanna Bojang na daktari wa timu, Kalifa Manneh.
Wachezaji waliopo ni Musa Camara, Abdou Jammeh, Momodou Futty Danso, Lamin Basmen Samateh, Ousman Koli, Pa Saikou Kujabi, Mustapha Kebba Jarju, Yankuba Mal Ceesay, Demba Savage, Saihou Gassama, Alieu Darboe, Momodou Ceesay, Pa Modou Jagne, Tijan Jaiteh, Bubacarr Sanyang, Christopher Allen, Musa Yaffa, Sulayman Marr, Mamut Saine, Hamsa Barry, Ali Sowe, Omar Colley na Saloum Faal.
Saa 4 kamili asubuhi ya leo kutakuwa na mkutano kati ya makocha wa timu zote mbili Kim Poulsen wa Taifa Stars na Luciano Mancini wa The Scorpions wakiwa na manahodha wao, Juma Kaseja “Taifa Stars” na Mustapha Jarju"Toubabo" mbele ya waandishi wa Habari utakaofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

No comments:

Post a Comment