VIEW OTHER SITES

Thursday

STARS,IVORY COAST KUPIGWA SAA 2 USIKU ZA AFRIKA MASHARIKI



Zikiwa zimebaki saa nne kabla kikosi cha timu ya taifa ya wanaume(soka) Taifa Stars kukwea pipa kuelekea Ivory Coast kwa mchezo wa kimataifa wa kufuzu fainali za kombe la dunia 2014 nchini Brazil timu hiyo itawakosa nyota wawili.

Stars yenye kikosi cha wachezaji 23 na viongozi 9 inatarajia kuondoka saa 11.10 alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kwenda Abidjan kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayochezwa Juni 2 mwaka huu.

Wachezaji walio kwenye orodha hiyo ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Nassor Masoud Cholo, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Waziri Salum, Shomari Kapombe na Juma Nyoso.

Wengine ni Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar, Shabani Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Haruna Moshi na John Bocco.

Wanaobaki kwa kuwa na majeruhi ni mshambuliaji Thomas Ulimwengu anayechezea klabu ya TP Englebert Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kiungo wa Yanga, Nurdin Bakari.

Viongozi wanaoondoka na timu ni Kocha Mkuu Kim Poulsen, Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Mukebezi (Meneja wa timu), Juma Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Daktari wa mifupa) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).

Msafara unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Crescentius Magori huku msaidizi wake akiwa Makamu wa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) Haji Ameir Haji.

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala akiwaaga wachezaji hao aliwataka kwenda kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye mchezo huo wakati wa hafla ya kukabidhi Bendera ya Taifa ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, Rais wa TFF, Leodegar Chilla Tenga na Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe ambao pia ni wadhamini wa Taifa Stars.

Mechi hiyo itachezwa saa 11 kamili kwa saa za Ivory Coast sawa na saa 2 kamili usiku Afrika Mashariki kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Felix Houphouet-Boigny aliyekuwa rais wa kwanza wa Ivory Coast ukichukua mashabiki 40,000.

Mwamuzi wa kati ni Slim Jedidi,mwamuzi msaidizi namba moja ni Bechir Hassani, wote kutoka Tunisia,mwamuzi msaidizi namba mbili ni Sherif Hassan kutoka Misri na mwamuzi wa akiba ni Youssef Essrayri pia kutoka Tunisia.

Mtathmini wa waamuzi ni Rachid Medjiba kutoka Algeria wakati Kamishna wa pambano hilo atakuwa Saleh Issa Mahamat kutoka Chad.

Stars itarajea nchini Juni 5 mwaka huu saa 1.40 asubuhi na kuingia kambini kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Gambia itakayochezwa Juni 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


No comments:

Post a Comment