SHIRIKISHO la Soka Tanzania nchini (TFF) limemtambulisha rasmi kocha mpya wa timu za Taifa za vijana, Jakob Michelsen kutoka Denmark hii leo mbele ya waandishi wa habari ambaye anachukua nafasi ya Kim Poulsen ambaye hivi sasa anakinoa kikosi cha wakubwa Taifa Stars.
Michelsen ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja alitambulishwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na kusema falsafa yake ni kama ile ya Poulsen ya kumiliki mpira na kushambulia muda wote wa mchezo.
Kabla ya ujio wake Tanzania, Michelsen alikuwa kocha wa timu ya daraja la kwanza ya Hobro IK ya Denmark. Ana leseni A ya ukocha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya ukocha wa vijana kutoka Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).
Moja ya mafanikio yake ni kuipa ubingwa wa Denmark, timu ya Skovbakken kwenye ligi ya timu zenye umri chini ya miaka 18. Ubingwa huo aliupata msimu wa 2005/2006.

No comments:
Post a Comment