VIEW OTHER SITES

Friday

RATIBA KAGAME YAWEKWA HADHARANI


MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame YANGA watafungua dimba na Atletico ya Burundi katika mchezo wa Kundi C wa michuano hiyo, Julai 14, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC waliowekwa Kundi A, wataanza na URA ya Uganda Julai 16, kwenye Uwanja huo huo.
Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo, Azam FC wao wataanza na Mafunzo ya Zanzibar katika mchezo wa Kundi B, Uwanja wa Chamazi, Julai 15.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholaus Musonye amesema katika Mkutano na Waandishi wa Habari mchana huu, ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam kwamba, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) itashiriki kama timu mualikwa.
Aidha,Musonye amesema Sudan, Ethiopia, Eritrea na Somalia hazitaleta wawakilishi wao kwa sababu mbalimbali.
Wakati, Ethiopia ligi yao inaanza wiki hii, Sudan wawakilishi wao wapo kwenye michuano ya Afrika na wameshindwa kuteua timu mbadala, Somalia wawakilishi wao Elman wamebadilisha uongozi, hivyo bado hawajajipanga na Eritrea kutokana na desturi ya wachezaji wao kuzamia kila wanapokuja kwenye mashindano, wameondolewa.
“Wameondolewa, kwa sababu mbili, kwanza nchi yao imeomba ipewe muda kulifanyia kazi sual hilo, na sisi pia (CECAFA) tunalitafutia ufumbuzi,”alisema Musonye.  
Lakini Musonye amekiri kitendo cha kuyatoa mashindano hayo mwanzoni mwa mwaka hadi katikati ya mwaka kumechangia baadhi ya timu kutoshiriki na amesema tayari amewasilisha pendekezo kwenye Mkutano Mkuu, mashindano yarejee kufanyika mwanzoni mwa mwaka kama ilivyokuwa awali.
Kuhusu mechi ya ufunguzi ya Simba kuchezwa Julai 16, ambayo itakuwa Jumatatu badala ya Jumapili, Musonye alisema kwamba imetokana na kwamba Julai 15, Uwanja wa Taifa kutakuwa na fainali za Copa Coca Cola, ambayo maandalizi yake yote yamekamilika.
Yanga ndiye bingwa mtetezi wa mashindano, baada ya kuifunga Simba SC katika fainali mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

RATIBA KAMILI KOMBE LA KAGAME

No comments:

Post a Comment